Skip to main content
ZLS receives the Legal Aid policy new edition - 2026 from the Minister of Constitution and Legal Affairs

Zanzibar Law Society (ZLS) yakutana na Waziri wa Katiba, Sheria, Utumishi na Utawala Bora – Zanzibar.

Chama cha Mawakili Zanzibar (ZLS), kikiongozwa na wajumbe wa Baraza lake la Uongozi—Mawakili Masoud Salim, Alphonce Gura, na Bi. Mufida Salum, wakiambatana na Mkurugenzi Mtendaji wa ZLS, Ndugu Shabani Seleman Mwangoda—kimefanya ziara ya kumtembelea Waziri wa Ofisi ya Rais – Katiba, Sheria, Utumishi na Utawala Bora, Mheshimiwa Dkt. Haroun Ali Suleiman.

Katika ziara hiyo, pamoja na kufikisha salamu za wanachama wa ZLS, ujumbe huo umehitimisha dhumuni la ziara kwa kuweka msisitizo katika kuimarisha na kuboresha mashirikiano ya karibu kati ya Chama na Wizara, hususani katika maeneo ya:

  • Kutoa Msaada wa Kisheria: Kuongeza fursa na upatikanaji wa huduma za msaada wa kisheria kwa wananchi wote wa Zanzibar
  • Marekebisho ya Sheria: Kufanya kazi kwa pamoja katika kufanya mapitio na marekebisho ya sheria mbalimbali nchini

     

Akizungumza katika kikao hicho, Mkurugenzi Mtendaji wa ZLS, Ndugu Shabani Seleman Mwangoda, alisema:

"Chama cha Mawakili Zanzibar kinaendelea kufanya maboresho makubwa ya kiutendaji na mifumo ndani ya taasisi. Kipo tayari na kimejiandaa ipasavyo kushirikiana na Idara ya Msaada wa Kisheria chini ya Wizara katika kuboresha upatikanaji wa huduma za msaada wa kisheria kwa wananchi wote wa Zanzibar, ikiwa ni pamoja na kuanzisha mfumo wa kidijitali wa maombi ya huduma hiyo kwa njia ya mtandao kupitia tovuti yao ya https://zls.or.tz/."

Akiunga mkono dhamira hiyo, Waziri wa Ofisi ya Rais – Katiba, Sheria, Utumishi na Utawala Bora, Mheshimiwa Dkt. Haroun Ali Suleiman, alisema:

"Nimefurahi na ninapongeza jitihada zote chanya za Chama cha Mawakili Zanzibar katika kuimarisha mashirikiano na Wizara, hususani katika maeneo ya huduma ya msaada wa kisheria kwa sababu huduma hii imelenga kuwafikia na kuwasaidia wananchi wanyonge, na kutolewa kwake kunachagiza maendeleo ya kiuchumi, kijamii na kisiasa. Ninasisitiza ushirikiano wa karibu zaidi na Chama cha Mawakili kwa kuongeza ushirikishwaji wao katika shughuli mbalimbali za Wizara."

Kwa upande wao wajumbe wa Baraza la Uongozi la ZLS walisisitiza utayari wao wa kufanya kazi kwa karibu na wizara katika maboresho ya sheria mbalimbali na kumualika Mh. Waziri kwenye Mkutano Mkuu wa mwaka wa Chama cha mawakili Afrika Mashariki (EALS) ambao unatarajiwa kufanyikia Zanzibar mnamo mwezi November 2026, ZLS akiwa mwenyeji wa Mkutano huo.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Idara ya Katiba na Msaada wa kisheria Wizarani, Bi. Hanifa R. Said, aliwahakikishia ZLS mshikamano thabiti katika maeneo hayo mawili, ambapo kwa kuanzia ameahidi kufufua jitihada za kuwa na Hati ya Makubaliano (MoU) na Chama cha Mawakili ili kurahisisha utendaji kazi wa pamoja.

Katika kuhitimisha ziara hiyo, Mheshimiwa Dkt. Haroun Ali Suleiman alimkabidhi nakala ya Sera Mpya ya Msaada wa Kisheria (Toleo la 2026) Mkurugenzi Mtendaji wa Chama Cha Mawakili Zanzibar (ZLS), Ndugu Shabani Seleman Mwangoda. 

Add new comment

Restricted HTML

  • You can align images (data-align="center"), but also videos, blockquotes, and so on.
  • You can caption images (data-caption="Text"), but also videos, blockquotes, and so on.

About

The Zanzibar Law Society is the statutory bar association of Zanzibar, established under the Zanzibar Law Society Act No. 7 of 2019 to uphold the rule of law and advance justice in Zanzibar.